Diana: Tanzanite tunaenda Poland kupambana
DAR ES SALAAM:NAHODHA wa timu ya taifa y… Read the rest
The post Diana: Tanzanite tunaenda Poland kupambana first appeared on SpotiLEO.
DAR ES SALAAM:NAHODHA wa timu ya taifa ya wanawake ya vijana, Tanzanite Queens, Diana Mnally amesema kikosi hicho kimejiandaa kikamilifu kwa ajili ya kushiriki Kombe la Dunia la Wanawake chini ya miaka 20 nchini Poland, kikilenga kwenda kupambana na timu zote kitakazokutana nazo.
Diana amesema wanafahamu ukubwa wa mashindano hayo na umuhimu wake, hivyo maandalizi yaliyofanyika yamejikita katika kuwajenga wachezaji kimwili na kisaikolojia ili wawe tayari kwa changamoto zitakazowakabili Poland.
“Mimi na timu nzima tumejiandaa vizuri kwa sababu tunajua ugumu wa mashindano haya. Ni mashindano makubwa ambayo huwa yanatokea mara chache, hivyo tunatambua uzito wake,” amesema Diana.
Nahodha huyo amesema baadhi ya wachezaji wa kikosi hicho wana uzoefu wa kushiriki mashindano ya dunia baada ya kuiwakilisha Tanzania mwaka 2022 katika Kombe la Dunia la Wanawake chini ya miaka 17, jambo analoamini litawasaidia wanapokwenda kushindana katika ngazi ya chini ya miaka 20.

Diana amesema walimu wao wamehakikisha wanawaandaa kwa kila upande, huku wakitambua kuwa watakutana na timu ambazo hawajawahi kucheza nazo wala kuziona kabla.
“Walimu wetu wametuandaa kisaikolojia na kimwili kwa ajili ya kwenda kushindana katika mashindano hayo. Sio mashindano madogo, ni makubwa na tutakutana na timu kubwa tofauti ambazo baadhi hatuzifahamu na hatujawahi kuziona,” amesema.
Amesema kutokana na hali hiyo, Tanzanite Queens itaingia kwenye mashindano hayo ikiwa na heshima kwa wapinzani wake, lakini bila kuwaogopa, wakilenga kutimiza malengo waliyojiwekea.
Katika hatua nyingine, Diana ameishukuru Serikali kwa namna ilivyokuwa ikikiunga mkono kikosi hicho katika maandalizi ya kuelekea mashindano hayo, akisema sapoti hiyo imekuwa chanzo cha faraja kwa wachezaji.
Tanzanite Queens inatarajiwa kuiwakilisha Tanzania katika Kombe la Dunia la Wanawake chini ya miaka 20 litakalofanyika nchini Poland, ikiwa ni hatua nyingine muhimu kwa maendeleo ya soka la wanawake nchini.
The post Diana: Tanzanite tunaenda Poland kupambana first appeared on SpotiLEO.
