August 31, 2026

DAR ES SALAAM: MWANAMUZIKI mkongwe wa Bongo Fleva na R&B, Banana Zoro, amewapongeza wasanii wa kizazi kipya wanaozingatia ubora wa kazi zao na wenye uwezo wa kuimba moja kwa moja bila kutegemea ‘playback’.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Spoti leo, Banana Zoro amesema miongoni mwa wasanii anaowakubali ni Nandy na Vanilla, kutokana na namna wanavyowasilisha kazi zao.

Aidha, amesema siri ya uimara wa bendi yake kwa miaka mingi ni nidhamu ya kazi, kuheshimu mikataba, kujenga uaminifu kwa mashabiki na kuwa na uhusiano mzuri na wanamuziki anaofanya nao kazi.

Banana Zoro amesema ukuaji wa mitandao ya kijamii umebadilisha kwa kiasi kikubwa tasnia ya muziki, kwani wasanii sasa wanaweza kuwafikia mashabiki moja kwa moja kupitia TikTok, Instagram na YouTube, tofauti na zamani walipotegemea zaidi redio na televisheni.

Hata hivyo, aliwataka wasanii chipukizi kuzingatia matumizi sahihi ya lugha katika utunzi ili kazi zao zidumu na kugusa vizazi vijavyo.

Amesema yeye na timu yake wanaendelea kusaidia vipaji vya vijana kwa lengo la kuibua kizazi kipya cha wasanii wa Bongo Fleva.

Banana Zoro pia anajihusisha na uigizaji, akiwa sehemu ya tamthilia ya Huba. Ni baba wa watoto watatu, wavulana wawili na msichana mmoja.

The post Banana Zoro awapongeza wasanii wanaoimba ‘live’ first appeared on SpotiLEO.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *