Yanga, Simba kazini leo
MBIO za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara … Read the rest
The post Yanga, Simba kazini leo first appeared on SpotiLEO.
MBIO za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara zinaendelea kushika kasi leo, huku macho yakielekezwa kwa vinara Yanga na Simba ambao wote wana pointi 12 baada ya kushinda michezo yao minne ya mwanzo.
Yanga inaongoza msimamo kwa tofauti ya mabao baada ya kufunga 13 na kuruhusu mawili, wakati Simba yenye pointi hizo hizo imefunga saba na kuruhusu mawili.
Mabingwa watetezi Yanga leo watakuwa ugenini kuikabili Fountain Gate kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, kuanzia saa 10:00 jioni, wakilenga ushindi utakaoendelea kuwaweka kileleni.
Yanga imeanza msimu kwa nguvu, ikiwa imeifunga Namungo 3-1, Coastal Union 4-1, JKT Tanzania 4-0 na Pamba Jiji 2-0, matokeo yaliyoifanya iwe na wastani mzuri wa ufungaji.

Fountain Gate, kwa upande mwingine, imepata ushindi mmoja pekee katika michezo minne, huku ikipoteza mitatu. Timu hiyo itatumia faida ya kucheza nyumbani kujaribu kuzuia kasi ya Yanga.
Rekodi pia zinaipa Yanga nafasi kubwa, kwani katika mechi nane zilizopita dhidi ya Fountain Gate, ambayo awali ilijulikana kama Singida Big Stars, Yanga imeshinda zote na kufunga mabao 24 huku ikiruhusu moja pekee.
Baada ya mchezo huo, Simba itashuka dimbani saa 12:30 jioni kuikaribisha Geita Gold kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ikiwa na lengo la kuendelea na mwanzo wake wa ushindi.
Simba imezishinda Kagera Sugar 2-0, Pamba Jiji 2-1, Singida Black Stars 2-1 na Coastal Union 1-0, huku ikiwa imeruhusu mabao mawili pekee katika michezo hiyo.
Geita Gold, ambayo imepanda daraja msimu huu, ina pointi saba baada ya kushinda mbili, sare moja na kupoteza mmoja, hivyo inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na matumaini ya kuwashtua wenyeji.
Rekodi za timu hizo zinaonesha Simba imeshinda michezo mitano kati ya sita ya Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold, huku mchezo mmoja ukiishia sare. Simba pia imefunga mabao 19 dhidi ya matatu ya Geita.
Mchezo mwingine ni kati ya Kagera Sugar na Azam FC kwenye Uwanja wa Kaitaba kuanzia saa 2:30 usiku. Azam ina pointi nane, wakati Kagera ikiwa mkiani kwa pointi moja, hivyo kila timu itahitaji matokeo mazuri kwa sababu tofauti.
The post Yanga, Simba kazini leo first appeared on SpotiLEO.
