September 3, 2026

ARUSHA: KOCHA wa TRA United, Etienne Ndayiragije, amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City kesho katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha, huku akiwataka wachezaji wake kutekeleza kwa ufanisi mipango waliyoiandaa katika mazoezi ili kupata matokeo wanayoyahitaji.

TRA United itakutana na Mbeya City, katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, huku kila upande ukihitaji matokeo mazuri katika harakati za kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi.

Ndayiragije amesema maandalizi yao yamejikita katika kuhakikisha wachezaji wanaelewa na kutekeleza falsafa ya timu pindi watakapoingia uwanjani.

“Tunajua umuhimu wa mchezo huu na tumejiandaa vizuri. Kitu muhimu ni kuona wachezaji wakitekeleza kile tulichokifanyia kazi katika mazoezi ili tupate matokeo tunayoyahitaji,” amesema Ndayiragije.

Kwa upande wake, nahodha wa TRA United, Nasr Kombo, amesema ushindi katika mchezo huo utakuwa muhimu kwa timu yao kwa kuongeza morali na kujiamini kwa wachezaji kuelekea michezo inayofuata.

Kwa upande wa Mbeya City, kocha Salim Mayanga amesema maandalizi yao yameenda vizuri na kikosi kipo katika hali nzuri, isipokuwa wachezaji wawili, Baraka Maranyingi na Aziz Kader, ambao watakosekana kutokana na majeraha.

Mayanga amesema licha ya kukabiliwa na changamoto hiyo, timu yake imejiandaa vizuri na inaamini wachezaji waliopo wataweza kutekeleza majukumu yao na kuipa timu matokeo mazuri.

Naye mchezaji wa Mbeya City, Baraka Maranyingi, amesema kikosi chao kina morali kubwa kuelekea mchezo huo na wachezaji wapo tayari kupambana kuhakikisha wanatimiza mipango waliyojiwekea.

The post TRA, Mbeya City kitawaka kesho first appeared on SpotiLEO.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *