September 2, 2026
Wasanii, Wanamtandao washiriki kikao na Katambi

DAR ES SALAAM: Wasanii na wanamtandao maarufu wamewasili katika kikao maalum kilichoitishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, huku ajenda rasmi za kikao hicho zikitarajiwa kuwekwa wazi leo.

Kikao hicho kimewakutanisha baadhi ya wasanii na watu maarufu wanaotengeneza maudhui mitandaoni, kufuatia mwito uliotolewa na Waziri Katambi kwa kundi hilo kuhudhuria mazungumzo hayo.

Miongoni mwa majina yaliyotajwa kuitwa katika kikao hicho ni Dudu Baya, Pipi Tida, Chidi Benzi, Lokole na Noel, pamoja na wengine. Orodha ya baadhi ya walioitwa ilisomwa jana na wasanii Gigy Money na Dotto Magari.

Hadi sasa, baadhi ya waliohudhuria wito ni Chidi Benzi, Q Chief, Maimartha Jesse, Mr Mwanya, Juma Lolote, Pipi Tida, Mwijaku, Stan Bakora, Masha Love na Gigy Money, pamoja na wengine walioitwa.

Hata hivyo, ajenda rasmi za kikao hicho bado hazijawekwa wazi.

Hali hiyo imeendelea kuibua mijadala miongoni mwa wadau wa burudani na mitandao ya kijamii kuhusu mambo yanayoweza kujadiliwa.

Baadhi ya wadau wanahusisha wito huo na masuala ya matumizi ya mitandao ya kijamii na maadili, ingawa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuthibitisha ajenda hizo.

Licha ya baadhi ya waliohudhuria kuonekana kuwa na hali ya tahadhari kuhusu wito huo, wengine wamewasili bila kuonyesha hofu, huku wakisubiri ufafanuzi kutoka kwa Waziri Katambi kuhusu lengo na masuala yatakayojadiliwa.

Kikao hicho kinatarajiwa kutoa picha zaidi kuhusu msimamo wa Serikali juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii, hususa kwa wasanii na watu wenye ushawishi mkubwa kwa jamii.

The post Wasanii, Wanamtandao washiriki kikao na Katambi first appeared on SpotiLEO.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *