September 1, 2026

DAR ES SALAAM: KATIKA safari ya muziki wa Bongo Fleva, yapo majina ambayo yameweza kujenga heshima kutokana na kipaji, ubunifu na uwezo wa kudumu katika mioyo ya mashabiki. Miongoni mwa majina hayo ni mwanamuziki Banana Zorro, anayekumbukwa kwa sauti yake ya kipekee na nyimbo zilizogusa maisha ya jamii.

Banana Zorro si jina geni katika tasnia ya muziki nchini. Katika mahojiano maalumu na Habari Leo Digital, msanii huyo anaeleza kuwa alianza kujihusisha na muziki akiwa kijana, akichochewa kwa kiasi kikubwa na mazingira ya familia yake yaliyokuwa yamezungukwa na sanaa.

Baba yake mzazi, Mzee Zahir Ally Zorro, alikuwa mwanamuziki anayeheshimika katika muziki wa dansi nchini Tanzania. Mazingira hayo yalimfanya Banana kukua akivutiwa na muziki na hatimaye kuamua kujenga safari yake mwenyewe katika tasnia hiyo.

Umaarufu wake uliongezeka baada ya kutoa wimbo “Mama Yangu”, uliopokelewa na mashabiki kutokana na ujumbe wake wa upendo, shukrani na kuthamini nafasi ya mama katika maisha.

Baada ya mafanikio hayo, aliendelea kutoa kazi mbalimbali zikiwamo “Nipo Radhi”, “Nzela”, “Mama Kumbena”, “Mapenzi Gani” na “Zoba”, ambazo zilionyesha uwezo wake wa kuimba na kuwasilisha hisia kupitia muziki.

Uwezo wa Banana Zorro kuchanganya ladha za R&B, Zouk na Bongo Fleva ulimfanya kuwa msanii mwenye mashabiki wa rika tofauti. Aidha, amefanya kazi mbalimbali na wasanii wengine, akichangia katika kukuza muziki wa kizazi kipya.

 

The post Banana Zorro: Sauti ya kipekee inayotikisa vipindi vyote first appeared on SpotiLEO.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *