September 1, 2026

DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI wa Simba, Ibrahim Doumbia, amesema makofi ya mashabiki baada ya mchezo yalimpa hisia kubwa, akieleza kuwa sapoti yao imeendelea kumtia nguvu licha ya kupitia kipindi kigumu.

Doumbia amesema baada ya kumalizika kwa mchezo huo, aliposikia mashabiki wakimshangilia na kumpigia makofi, alipata tena hisia zile alizozipata aliposhuka kwenye basi na kukutana na bango lenye ujumbe wa kumtia moyo.

Kauli yake hiyo inakuja baada ya kuwepo kwa kelele nyingi mitandaoni ya kubeza kiwango chake tangu kujiunga na wekundu hao.

Katika ujumbe wake alioutoa jana kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii, amesema kitendo cha mashabiki wa Simba kumuunga mkono kimemfanya atambue zaidi kuwa wapo pamoja naye, hasa katika kipindi ambacho amekuwa akikabiliwa na changamoto mbalimbali.

“Baada ya mchezo, niliposikia makofi yenu, nilihisi hisia zilezile. Licha ya kila kitu kinachotokea, upendo na sapoti yenu vina maana kubwa kwangu,” amesema Doumbia.

Amesema ataendelea kufanya kazi kwa bidii, kujifunza na kuboresha kiwango chake, akisisitiza kuwa lengo lake ni kuwapa mashabiki sababu zaidi za kufurahia uwanjani.

Doumbia pia amewataka mashabiki wa Simba kuendelea kuwa na imani naye, akiahidi kupambana kwa ajili ya jezi hiyo na kulipa sapoti wanayompa kupitia matokeo mazuri ndani ya uwanja.

“Sitaki kuzungumza sana, nataka kufanya kazi, kujifunza, kuboresha na kupambana. Zaidi ya yote, nataka kulipa upendo wenu ndani ya uwanja,” amesema.

 

The post Doumbia aguswa na sapoti ya mashabiki Simba first appeared on SpotiLEO.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *